Rais wa Tanzania John Magufuli aongoza salamu za rambirambi msiba wa Mengi

Posted on by ERICK MWEMUTSI

Mwenyekiti wa makampuni ya IPP na moja ya watu matajiri na mashuhuri nchini Tanzania Reginald Mengi amefariki dunia.

Taarifa hiyo imethibitishwa leo alfajiri na vyombo vya habari vilivyo chini ya umiliki wake, runinga ya ITV, na stesheni ya Radio ONE.

Mzee Mengi alizaliwa mwaka 1944 mkoani Kilimanjaro na umauti umemkuta akiwa mjini Dubai, Falme za Kiarabu baada ya kuugua kwa muda mfupi, kwa mujibu wa familia yake.

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli, ameongoza mamilioni ya Watanzania kutuma salamu za rambirambi kufuatia msiba huo.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa Twitter Magufuli amesema ataendelea kumkumbuka Mzee Mengi kwa mchango wake katika maendeleo ya taifa lake.

Salamu za rambirambi pia zimetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania Dkt Hassan Abbas ambaye amenukuu kauli ya marehemu Mengi kuwa; ” ‘watu wanaoacha alama hawafi’, basi mawazo, falsafa, ubunifu na kujitoa kwake vitaendelea kuishi nasi.”

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania pia umetoa tamko kupitia itandao ya kijamii na kuelezea kusikitishwa na taarifa hizo za msiba.

Mwakilishi Mkaazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, Alvaro Rodriguez pia ametuma salamu zake za rambirambi.

Waziri wa zamani wa Habari nchini Tanzania Nape Nnauye naye ametumia ukurasa wake wa Twitter kuelezea masikitiko yake juu ya kifo cha mtu aliyemuita kuwa ni ‘rafiki, mshakaji, kiongozi na mzazi.’
“Ulinifundisha kuwa kukata tamaa ni dhambi,” ameandika Nnauye.

Mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania Mohammed Dewji pia ametuma salamu zake za rambi ambi akimtakia kheri marehemu.

About the Author

Leave A Response