MBOWE: SIPENDI UNAFIKI; KWAMBA KUNA MAKABILA HAYAWEZI KUSAIDIA WALEMAVU!

Posted on by ERICK MWEMUTSI

MWENYEKITI  wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amewataka Watanzania kutogombanishwa na kauli za viongozi hasa za kikabila na kidini huku akiwataka viongozi kutafakari maneno kabla ya kuyaongea kwani yanaweza kugawa watu na kuleta machafuko.

Aidha, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, amesema aliyekuwa Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dkt. Reginald Mengi alikuwa  mtu asiyekata tamaa.

Mbowe ameyasema hayo Mei 9, alipokuwa akitoa salamu za rambirambi katika ibada ya kumuaga  Mengi iliyofanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Moshi Mjini mkoani Kilimanjaro.

“Kuna kauli zinasemwa sana watu na kwa ukweli zinakera kwa vile mimi si mnafiki lazima niseme na nitasema hapahapa mbele za watu.

“Tuna nchi moja ambayo tunastahili kupendana na kusaidiana, na kila mtu ana haki ya kumsaidia mwenzie, tusikubali kauli za viongozi zitugawe na hasa za kidini na kikabila, kauli ya kusema kuna makabila hayawezi kuwasaidia walemavu si nzuri na haikutupendeza kwa kweli, tujitafakari tunapotaka kuongea maneno,” amesema Mbowe.

Aidha Mbowe ametoa wito kwa kila aliyeguswa na msiba wa Mengi kuyaenzi yale yate aliyokuwa akiyatenda enzi za uhai wake kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kumuenzi.

“Mzee Mengi ameshatangulia mbele za haki haitajalisha tuzungumze mema kiasi gani kuhusu yeye kwani hatutamrejesha, ila tujitafakari na kuyaenzi yale aliyokuwa akiyafanya, alikuwa mnyeyekevu na kauli zake zilijenga, kupatanisha na kuleta matumaini lakini pia hakuwahi kukata tamaa,” amesema Mbowe.

About the Author

Leave A Response