MEMBE: DKT MENGI ALINIPIGA TAFU KWENYE MBIO ZA URAIS 2015

Posted on by ERICK MWEMUTSI
ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, amesema aliyekuwa Mwenyekiti wa Makampuni ya IPP Limited, marehemu Reginald Mengi alimuunga mkono katika jitihada zake za kutafuta urais mwaka 2015.
“Niseme tu hakuwa mbaguzi, aliunga mkono kila mtu aliyekuwa na nia ya kugombea urais na aliwasaidia, wengine walikataa, mimi nakubali alinisaidia.
“Mtakumbuka Watanzania,  Somalia ilipopatwa na tatizo la njaa iliyowakabili watu milioni 10 mwaka 2009/10 Rais Jakaya Mrisho Kikwete alimteua Dkt. Reginald Mengi kuwa mwenyekti wa wafanyabiashara wote ambao walitakiwa kuchanga na kuichangia Somalia. Dkt Mengi alifanya kazi kubwa akisaidiana na wizara ya mambo ya nchi za nje kupata michango mbalimbali.
“Alifanya kazi nzuri tukapata malori kadhaa ambayo yalipeleka chakula moja kwa moja Somalia kupitia Kenya,” amesema Membe, na kuongeza kuwa amepoteza mtu aliyekuwa rafiki wa familia yake kwa zaidi ya miaka 12.
Mwili wa Dkt. Mengi unaagwa leo Mei 9, katika Kanisa la KKKT Usharika wa Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro na baadaye kuzikwa Machame.
About the Author

Leave A Response