SHAMIM NA MUMEWE WAFIKISHWA KORTINI

Posted on by ERICK MWEMUTSI

MFANYABIASHARA Abdul Nsembo ‘Abdukandida’ (45) na mkewe Shamim Mwasha (41) ambao ni wakazi wa Mbezi Beach jijini Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Jumatatu, Mei 13, 2019 wakikabiliwa na kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 232.70.

Akisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kelvin Mhina, wakili wa Serikali, Costantine Kakula, amedai kuwa kosa lao ni la uhujumu uchumi. Amesema Mei Mosi mwaka huu, washtakiwa hao kwa pamoja wakiwa maeneo ya Mbezi Beach walisafirisha dawa za kulevya zenye uzito wa gramu 232.70 huku wakijua kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Kakula alisema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na aliiomba mahakama hiyo ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuisikiliza.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo Hakimu Mhina alisema washtakiwa hao hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa kosa wanaloshtakiwa ni la uhujumu uchumi hivyo mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo na kwamba hawana dhamana.

Wakili wa utetezi, Hajra Mungula,  aliuomba upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi ili hatua nyingine ziweze kuendelea. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27, 2019 itakapotajwa tena.

About the Author

Leave A Response